Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kimataifa ya Kanda ya tatu ya mchezo wa ngumi yanayotarajiwa kufanyika Aprili 18 hadi 23, mwaka huu, katika Uwanja wa ndani wa Mkapa, Dar es Salaam.
Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), Lusekelo Willilo, amesema maandalizi ya michuano ipo katika hatua za mwisho na timu ya Taifa ya Tanzania ipo kambini kujiandaa na mashindano.
Willilo amesema Tanzania itawakilishwa na mabondia 32 wakiwemo wa timu mbili za wanaume na mmoja ya wanawake.
Wililo amezitaja nchi zilizothibisha kushiriki mashindano hayo kuwa ni Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Cameroon na mwenyeji Tanzania.
Amesema Rwanda, Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo DRC na Gabon zinatarajiwa kushiriki pamoja na kutothibitisha ushiriki wao hadi sasa.
Nahodha ya timu ya Tanzania, Yusuph Changalawe, amesema maandalizi yanaendelea vizuri na wamejipanga kupeperusha vyema bendera ya nchi na kuutumia uenyeji kuvuna medali na kutwaa ushindi wa jumla.