Tanzania na Liechtenstein zimekubaliana kuweka mpango mkakati wa kuwekeza katika kilimo hai na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo katika mikoa ya Morogogo na Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler ambaye yuko nchi kwa ziara ya kikazi.
Katika mazungumzo hayo viongozi hao wamekubalia kuangazia maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za Utalii, Viwanda, na Elimu, hususan kumuendeleza mtoto wa kike katika masomo ya sayansi na teknolojia.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Dominique Hasler amesema Liechtenstein ina uhusiano imara na wa siku nyingi na Tanzania na kwamba Nchi yake imekuwa kisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo hapa nchini hivyo uwepo wake ni wa nia ya kuiona miradi hiyo na kujadiliana namna bora ya kuiendeleza.
Waziri Hasler akiwa nchini atatembelea miradi mbalimbali ya kilimo hai inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Liechtenstein kupitia Sustainable Agriculture Tanzania (SAT) katika mkoa wa Morogoro na Dodoma.