Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani, Mfuko wa Mabadiliko tabia nchi (CGF) na wananchi, imetenga kiasi cha shilingi bilioni 375.4  kutekeleza Mradi wa kukabiliana na changamoto  zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi mkoani Simiyu kwa awamu ya kwanza, ambao utakuwa suluhisho la kudumu la tatizo la maji mkoani humo

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi, Isack Kamwelwe wakati akifungua kikao cha wadau wa mabadiliko ya tabia nchi kilichofanyika Mjini Bariadi Mkoani Simiyu.

Amesema kuwa moja ya shughuli muhimu na kubwa katika utekelezaji wa Mradi wa kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi, ni ufikishaji wa huduma ya Maji ya Ziwa Victoria katika Mji wa Bariadi, Busega na Itilima kwa awamu ya kwanza na baadaye katika Wilaya ya Meatu na Maswa.

Aidha, ameongeza kuwa upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Simiyu uko chini ikilinganishwa na wastani wa Kitaifa na kwa kutambua hali hiyo,  Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ilibuni mradi huo, ili kupata suluhisho la kudumu  la tatizo la maji kwa wananchi na mifugo ambayo ni moja ya shughuli za kiuchumi za wananchi wa Mkoa wa huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka ameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo ambao utawasaidia wananchi wa mkoa huo na utakuwa chachu katika Ujenzi wa Viwanda mkoani humo kwa kuwezesha upatikanaji wa maji ya uhakika.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Profesa, Kitila Mkumbo amesema kuwa Simiyu ni Miongoni mwa Mikoa yenye kiwango cha chini cha upatikanaji wa huduma ya maji ambayo Serikali imetoa kiupaumbele cha kuipa fedha kutoka katika Fedha za Mfuko wa Maji ili kutekeleza miradi ya maji itakayoibuliwa na kuwasilisha maandiko yake wizarani.

 

Tanesco yawaomba radhi wateja wake
Magazeti ya Tanzania leo Novemba 30, 2017