Serikali ya Tanzania na ya Namibia zajidhatiti kukuza na kuendeleza kiwango cha biashara na uchumi kwa kutumia rasirimali zinazopatikana kati ya mataifa hayo.
Makubaliano hayo yamefikiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah wakati wa kuhitimisha Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya nchi hizo jijini Dar es Salaam.
Prof. Kabudi amesema kuwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Namibia bado ni kidogo kikilinganishwa na fursa zilizopo, licha ya kiwango hicho kukua kutoka shilingi milioni 2,562.81 kwa mwaka 2010 hadi shilingi milioni 21,830.3 kwa mwaka 2018.
Kutokana na takwimu hizo, Prof. Kabudi amesema ni dhahiri kwamba Mamlaka husika zinatakiwa kufanya jitihada za kutosha kwa kuhamasisha na kukuza uwekezaji baina ya nchi hizo. Aidha, pamoja na mambo mengine, Prof. Kabudi ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Namibia kuja kuwekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo, sekta ya mafuta na gesi, kilimo na biashara, viwanda vya dawa, ujenzi na utalii pamoja na uvuvi.
“Serikali ya Tanzania inafanya jitihada mbalimbali za kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini ili kuhakikisha kuwa wawekezaji wanawekeza mahali salama. Jitihada hizo ni pamoja na utekelezaji wa blue print ambao unasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji,” amesema Prof. Kabudi.
Ameongeza kuwa kutokana na jitihada hizo, ripoti ya Benki ya Rand Merchant ya Afrika Kusini imeonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya saba (7) bora kwa uwekezaji kati ya nchi 52 za Afrika. Aidha, ripoti ya The African Index (AII) 2018 imeonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 13 kati ya nchi 54 kwa kuwa na masoko na vivutio vya utalii.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na kwamba ushirikiano wa Namibia na Tanzania ni wa kindugu, kidiplomasia, kiuchumi na ni wa kudumu.
“Napenda kutumia fursa hii kuwasihi sana wafanyabiashara kutoka nchini Namibia na Tanzania kushirkiana na kuona namna ya kukuza sekta ya biashara, utalii, kilimo, viwanda vya dawa, ujenzi pamoja na uvuvi kwani kupitia uwekezaji huo tutaweza kukuza kiwango cha mapato kati ya mataifa yetu,” amesema Nandi-Ndaitwah.
Katika mkutano huo, nchi hizo zimekubaliana kuendeleza ushirikiano katika Utamaduni, Sanaa na Michezo; Ushirikiano katika sekta ya Utalii pamoja na ushirikiano kwenye maendeleo ya vijana. Katika maeneo mengine, majadiliano yanaendelea na pande hizo mbili zimekubaliana hadi kufikia mwezi Machi 2020, Hati za Makubaliano ziwe zimesainiwa katika maeneo hayo.
Mkutano huo wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Namibia ulianza katika ngazi ya maafisa waandamizi wa Serikali na kufuatiwa na ngazi ya Makatibu Wakuu na kuhitimishwa na Mawaziri wa Mambo ya nje jana jijini Dar es Salaam.