Kikosi cha Maafande wa Jeshi la Magereza ‘Tanzania Prisons’ kimetangaza hali ya hatari kwa Azam FC kuelekea mchezo wa mzunguuko watano wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaopigwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokione jijini Mbeya Septemba 30.
Tanzania Prisons watashuka dimbani siku hiyo wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza nyumbani dhidi ya Simba SC, huku Azam FC wakiwa na shangwe la kuibamiza Mbeya City ugenini.
Afisa Habari wa Tanzania Prisons Luka Mwafulango wamesema kikosi chao kinaendelea kujiandaa na mchezo huo, huku kikiwa na matumaini makubwa ya kurejesha furaha kwa mashabiki wake, baada yakushindwa kufurukuta dhidi ya Simba SC.
“Kikosi kinaendelea na maandalizi ya mchezo wetu dhidi ya Azam FC, wachezaji wana ari kubwa ya kupambana na kupata ushindi siku ya Ijumaa ya juma lijalo, hatutahitaji tena kuona mashabiki wetu wakiingia simanzi kama ilivyokua katika mchezo wetu wa mwisho dhidi ya Simba SC.”
“Tunafahami Azam FC wana timu nzuri, itatupa upinzani mkali katika mchezo huo, lakini lengo letu ni kuhakikisha tunabakisha alama tatu nyumbani siku hiyo,”
“Katika siku kadhaa zilizosalia kabla ya kukutana na Azam FC, Benchi la Ufundi limependekeza kikosi chetu kicheze mchezo ya kirafiki huko Kyela, Siku ya Jumapili tutacheza mchezo wetu wa kwanza kisha tutarejea Mbeya mjini kwa mchezo mwingine na badaa ya hapo tutacheza dhidi ya Azam FC.” amesema Mwafulango
Wakati Tanzania Prisons wakijiandaa jijini Mbeya, Azam FC wapo mjini Ndola-Zambia wakicheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki leo Ijumaa (Septemba 23), dhidi ya Mabingwa mara tano wa Afrika TP Mazembe.