Kocha msaidizi wa Tanzania Prisons, Shaban Kazumba amefichua siri ya kuibana Young Africans kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21, uliochezwa jana Usiku Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.
Young Africans ambao walikua nyumbani jana Jumapili, waliambulia matokeo ya sare ya bao moja kwa moja dhidi ya wapinzani wao kutoka jijini Mbeya, lakini kwa msimu huu wamejinasibu kuutumia uwanja wa Nelson Mandela wa mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, kama uwanja wao wa nyumbani.
Kazumba amesema matokeo ya mchezo dhidi ya Young Africans walianza kuyaanda kwa kipindi kirefu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu, na walidhamiria kuwafunga, lakini kwa bahati mbaya waliambulia alama moja.
Amesema benchi la ufundi la Tanzania Prisons linaloongozwa na kocha Salum Mayanga walibaini baadhi ya mbinu za Young Africans, kupitia mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Eagle Noir, uliochezwa Agosti 30.
“Tulibaini wachezaji hatari wa Young Africans wakati walipokuwa wanashambulia na kuona mapungufu ya kuyatumia wakati wa tunapokwenda kuwashambulia na hayo ndio tuliyatumia,” amesema.
“Tulibaini Young Africans hawana utimamu wa mwili (FIT) wa kutosha na tuliwandaa wachezaji wetu katika hali hiyo lakini hata mfumo wetu wa 4-5-1, ulifanikiwa kwa kila mchezaji kwenda kufanya kazi yake.
“Timu yetu ukingalia ile ambayo tulimaliza nayo msimu ndio tumebaki nayo wachezaji wawili tu ndio wameondoka na tumeongeza wachache kama Mohammed Mkopi kulingana na mapungufu yetu,” amesema Kazumba.
“Ukiangalia msimu uliopita tulianza na rekodi nzuri ya kutokupoteza michezo ya mwanzo jambo ambalo tunataka kuliendeleza pia kwenye msimu huu,” ameongezea Kazumba.