Ujumbe wa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo Saidi Yakubu wamekutana na kufanya kikao pamoja na Balozi wa Qatar hapa nchini Hussain Ahmad kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mashindano ya Kombe la Dunia linalosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).
Viongozi hao wamefanya kikao cha pamoja Juni 23, 2022 katika Ofisi za Ubalozi wa Qatar hapa nchini Oyster Bay jijini Dar es Salaam kwa kuwa Mashindano ya Kombe la Dunia yatafanyika nchini Qatar mwaka huu 2022.
Katika mazungumzo yao viongozi hao wamekubaliana pande zote mbili kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo kutumia wataalamu wa Tanzania kushiriki maandalizi kabla, wakati na baada ya mashindano hayo ikiwa ni fursa adhimu kwa Tanzania kujifunza namna ya kuandaa mashindano ya kimataifa.
Naibu Katibu Mkuu, Yakubu pia amewasilisha kwa Balozi huyo maombi ya vijana wa Tanzania kupata fursa ya ajira za muda wakati wa mashindano hayo yatakayofanyika nchini Qatar.
Aidha, katika mazungumzo yao Naibu Katibu Yakubu ametumia fursa hiyo kumkaribisha Balozi wa Qatar hapa nchini Hussain Ahmad kushiriki kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ambayo yanaadhimishwa kwa mara ya kwanza duniani baada ya kuidhinishwa na Mkutano Mkuu wa 41 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Novemba 23, 2021 ulipitisha azimio namba 41C/61 la kutangaza tarehe 7 mwezi Julai kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani.
Katika maadhimisho hayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi ambapo siku hiyo itaadhimishwa kuudhihirishia ulimwengu kuwa asili ya lugha ya Kiswahili ni Tanzania.
Kwa upande wake Balozi Hussain amesema amepokea maombi hayo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa kuzingatia uhusiano na ushirikiano mzuri uliyopo baina ya nchi hizo mbili.