Rwanda imesema ipo tayari kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania, hasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Kauli hiyo imetolewa na Rais Paul Kagame wa Rwanda katika ujumbe wake uliowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu Chamwino mkoani Dodoma na Mjumbe Maalum na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa nchi hiyo Dkt. Vincent Biruta.

Katika ujumbe huo Rais Kagame amesema kuwa Rwanda itakuza zaidi ushirikiano na Tanzania katika utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa Rusumo na ujenzi wa reli ya kisasa ya kuunganisha jiji la Kigali nchini Rwanda na Isaka nchini Tanzania, miradi ambayo itasaidia usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda nchini Rwanda.

Rais Kagame katika ujumbe wake pia ametuma salamu za pole kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Magufuli na amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupokea kijiti cha Urais.

Kwa upande wake Rais Samia Suluhu Hassan amemshukuru Rais Kagame kwa kumtumia ujumbe huo uliojumuisha salamu za pole na pongezi na amemhakikishia kuwa Tanzania ipo tayari kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Rwanda.

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya pamoja, ametaka Tume ya Pamoja ya Ushirikiano wa Tanzania na Rwanda (JPC) ikutane ili kuongeza msukumo katika miradi hiyo pamoja na kuainisha maeneo mapya ya ushirikiano yenye maslahi kwa pande zote mbili.

Maeneo mengine ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ametaka JPC ifanyie kazi, ni kuimarisha usafirishaji wa minofu ya samaki kutoka Mwanza kwa kutumia Shirika la Ndege la Rwanda na kuharakisha ujenzi wa bandari kavu ya Isaka.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Juni 4, 2021
Masau Bwire: Simba SC ilituzidi