Baada ya kuiondoa Sudan Kusini katika mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza wa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika chini ya Umri wa miaka 23, Timu ya taifa ya Tanzania itakutana na Nigeria mwezi Oktoba.
Mchezo huo wa Mzunguuko wa Pili wa kuwania kufuzu Fainali za AFCON zitakazounguruma mwaka 2023 nchini Morocco, Tanzania itaanzia nyumbani Oktoba 20, `na juma moja baadae (Oktoba 27) itakwenda ugenini Nigeria.
Mshindi wa jumla wa mchezo huo, atakutana na Mshindi wa jumla wa mchezo kati ya Guinea dhidi ya Uganda, mwezi Machi mwaka 2023.
Mshindi wa jumla wa mchezo huo atafuzu moja kwa moja kwenye Fainali za Afrika (AFCON U23), zilizopangwa kuanza kurindima nchini Morocco Mwezi Juni 2023.
Tanzania imefuzu kucheza Mzunguuko wa Pili kwa kunufaika na bao la ugenini, kufuatia matokeo ya sare ya 3-3 dhidi ya Sudan Kusini yaliyopatikana jana Jumatatu (Septemba 26) nchini Rwanda.
Mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa Uwanja wa Azam Complex-Chamazi jijini Dar es salaam, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.