Wakimbizi wa Burundi 600 waliokimbilia nchini Tanzania wamerudishwa makwao “kwa hiari yao” tangu Alhamisi, Oktoba 3 kwa mujibu wa serikali ya Tanzania.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi, UNHCR, lilikuwa limepanga siku za hivi karibuni kuwarudisha Burundi wakimbizi takribani 400, wote kwa hiari yao.

Hata hivyo wakimbizi 588 ndio walisafirishwa hadi katika kambi ya muda ya Nyabitare katika mkoa wa Ruyigi, mashariki mwa Burundi.

Huku UNHCR ikihakikisha kwamba inachunguza kuwa ale ambao waliongezwa katika kundi hilo la watu 400 wamerudishwa kwa hiari yao.

Tangu mwaka 2017, wakimbizi zaidi ya 78,000 kutoka Burundi wamerudishwa kutoka Tanzania.

Waziri wa Mambo ya ndani Tanzania alitangaza kwamba serikali yake itawarudisha kwa hiari yao au kwa nguvu wakimbizi wote wa Burundi kuanzia Oktoba mosi  mwaka huu ambapo uamuzi huo ulikosolewa na jamii ya kimataifa.

Lakini siku ya Alhamisi asubuhi serikali ya Tanzania ilibadili msimamo na kurejelea kauli yake.

Ambapo Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Hassan Abbas, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam alibaini kwamba “hakuna mkimbizi wa Burundi atalazimishwa kurudi nchini mwake, kama sio kwa hiari yake”.

Katika kambi ya wakimbizi ya Nduta, Gerard, ambaye alitoroka nchi yake ya Burundi tangu kuzuka kwa mgogoro wa kisaisa wa mwaka 2015, alisema kwamba anafurahishwa na kauli hiyo ya serikali ya Tanzania, lakini ana matumaini kwamba “viongozi wa Tanzania hawatabadili tena kauli hiyo”.
Wakimbizi 588 waliorudishwa nchini Burundi wanatarajia kusafirishwa hadi katika vijiji vyao leo Ijumaa.

Bado kuna wakimbizi wa Burundi 225,000 nchini Tanzania, wakati maelfu ya Warundi wanaendelea kuitoroka nchi yao kila mwezi, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi, UNHCR.

Isaac Promise afariki dunia, Ferdinand amlilia
Southgate atangaza kikosi kitakachozivaa Jamuhuri ya Czech, Bulgaria