Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imethibitisha kuongezeka kwa wagonjwa wapya wanne wa maambukizi ya virusi vya Corona (COVID -19).
Ambapo Tanzania bara wamepatikana wagonjwa wawili kutoka jiji la Dar es salaam na Mwanza huku wagonjwa wengine wawili walitangazwa na Waziri wa Afya wa Zanizibar Jana Machi 5, 2020 na kufanya hadi sasa Tanzania kuwapo kwa jumla ya kesi 24 zilizoripotiwa tangu kuanza kwa ugonjwa huu nchini.
Mgonjwa wa Kwanza kutoka Tanzania Bara ni Mwanaume mwenye umri wa miaka 41 raia wa Tanzania na mfanyabiashara mkazi wa Mwanza aliyeingia nchini kutoka Dubai Tarehe 24 Machi, 2020 kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere (JNIA) na kuelekea Mwanza tarehe Machi 29,2020 ambapo alichukuliwa vipimo na kukutwa na maambukizi ya virusi vya Corona, Taarifa imeeleza hivyo.
Na mgonjwa mwingine kutoka Tanzania Bara ni mwanaume mwenye umri wa miaka 35 raia wa Tanzania mkazi wa Dar es salaam ambae pia ni mfanyabiashara.
Wizara imesema tayari wagonjwa wote wapo karantini chini ya uangalizi wa watoa huduma za afya katika vituo maalum vya tiba Dar es salaam, Zanzibar na Mwanza.
Aidha Serikali inaendelea kutoa msisitizo juu ya wananchi kufuata taratibu za kujikinga dhidi ya virusi hivi vya Corona.