Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema hadi sasa jumla ya Wagonjwa waliopona virusi vya Corona wafikia 48 ambao ni kati ya Wagonjwa 108 waliothibitika kuwa na Ugonjwa huo.
Ambapo leo wameruhusu watu 37, na kuwa vipimo vyao vimeonesha hawana maambukizi ya COVID19 na watu 11 walishatolewa taarifa kuwa wamepona na waliruhusiwa.
Amesma takwimu iliyopo sasa ni kwamba Tanzania ina jumla ya vifo 10, na idadi ya wagonjwa waliobaki ni 274 .
”Ni kweli kama alivyosema Rais Magufuli katika watu 263 waliobaki, 108 hawana ugonjwa wowote” Amesema Waziri Ummy.
Ameongeza kuwa watu hao 108 hawana homa, kifua, kikohozi wala chochote, ila walizuiliwa kubaki katika kituo kwa ajili ya vipimo vya mwisho na kuthibitisha kama hawana maambukizi kabla ya kuwaruhusu kwenda nyumbani.
“Jumla ya watu waliopata maambukizi nchini ni 284, vifo ni 10 na hivyo tukabakiwa na watu 274 na kati ya hao 11 tulishawatolea taarifa kwamba wamepona na kati ya watu 263 watu 108, hawana ugonjwa wowote, kwahiyo leo hii tumewaruhusu watu 37 wameenda nyumbani tusiwanyanyapae ni ndugu zetu, lakini nitoe angalizo hata kama umepona Corona unaweza ukapata tena maambukizi, hivyo niwaombe wajilinde na kujikinga“ amesema Waziri Ummy.
Ametoa wito kwa jamii kuwa isiwanyanyapae na kuongeza kuwa wengine 71 vipimo vyao vinasubiri siku 2-3 wataruhusiwa kurudi nyumbani.
Aidha pia amewataka wale wote walioruhusiwa baada ya kupona waendelee kuchukua tahadhari ili wasipate maambukizi mengine kwani tafiti zilizofanyika kuhusu hiki kirusi zinaonyesha kuwa mtu akipona ugonjwa huo anaweza kuupata tena, hivyo amewapa tahadhari hiyo na kuwataka waendelea kufuata maelekezo yanayotolewa n awatalaamu wa afya juu ya kujikinga na Corona.