Neema Mbuja – Kampala, Uganda.
Serikali ya Tanzania, imeahidi kuendeleza Ushirikiano, Umoja na Mshikamano na Uganda kwa manufaa ya nchi zote mbili kutokana na historia iliyoanza tangu kipindi cha harakati za Uhuru baina ya waasisi wa Mataifa haya na ushirikiano unaoendelezwa ikiwemo kudumishwa kwa umoja, amani, mshikamano na utu.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameyasema hayo wakati akiwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru wa Uganda, yaliyofanyika Oktoba 9, 2023.
Alisema, Rais Dkt. Samia anathamini mchango na maendeleo yaliyofikiwa na nchi ya Uganda katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi, huku akimshukuru Rais Yoweri Museveni kwa jitihada zake za kudumisha umoja na mshikamano kwenye jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hafla hiyo ya Miaka 61 ya Uhuru wa Uganda, ilihudhuriwa na Makamu wa Rais Burundi, Prosper Bazombanza, Wawakilishi kutoka Jumuiya ya falme za kiarabu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Kenya, Peter Mathuki, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini Uganda, Mawaziri, Viongozi mbalimbali wa Taifa hilo na Wananchi.