Kampuni ya Afrika General Chamber of Commerce imeandaa maonyesho ya biashara ya vipodozi yatakayofanyika nchini China mwezi March mwaka huu.
Katika maonyesho hayo Tanzania imepewa mwaliko wa kushiriki ambapo wadau wa vipodozi wametakiwa kuchangamkia fursa ya biashara kati ya Tanzania na China.
Makamu wa rais wa kampuni hiyo, Rex Chan amesema kuwa tangu mwaka 2005 China imekuwa mshirika mkubwa wa kibiashara barani Afrika na kutokana na utafiti wao wamegundua Afrika kuna soko kubwa la vipodozi.
Aidha, Chan ameeleza kuwa milango ipo wazi kwa wafanyabiashara ambao ni watengeneza vipodozi kushiriki maonyesho na kampuni hiyo itagharamia usafiri kwa wafanyabiashara watakaopenda kushiriki.
“kampuni yetu imekuwa ikijihusisha na masuala ya vipodozi halisi, tumeamua kuja kuwekeza Tanzania kutokana na biashara hii kukua kwa wingi, hivyo kwa atakayehitaji kushiriki apige simu namba +85228112862 ili agharamiwe usafiri,”amesema Chan
Kwa upande wa Mkurugenzi msaidizi wa waandaaji wa maonyesho hayo, Haifan Zhang amesema kuwa maonyesho yatawapa fursa ya kukutana na wataalamu waliobobea kwenye viwanda na kufungua milango ya soko la bidhaa zao.
Hata hivyo, maonyesho hayo yatahusu bidhaa kama vile za saluni, urembo na zinazotibu mikunjo, bidhaa za tatuu, za afya za jadi za kupunguza uzito na kutakuwa na mafunzo ya elimu ya ngozi.