Tanzania inashiriki mkutano wa 74 wa Kamati Kuu ya Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyamapori na Mimea Iliyo hatarini kutoweka (CITES) unaoendelea Lyon, Rhone-Alpes nchini Ufaransa.
Mkutano huo uliofunguliwa na Waziri wa Usafirishaji na Bioanuai wa Ufaransa, Barbara Pompili, umehudhuriwa na washiriki zaidi ya 500 kutoka nchi 183 wanachamana wa Mkataba wa CITES.
Mkutano huo unajadili masuala mbalimbali yanayohusu uendeshaji wa Mkataba, mpango wa uendeshaji wa Mkataba, masuala ya kimkakati ya uhifadhi, tafsiri ya utekelezaji wa Mkataba na masuala mahususi ya spishi huku jumla ya hoja 89 zikijadiliwa ambapo Tanzania imetoa mchango katika hoja 40 zenye maslahi kwa uhifadhi wa wanyamapori na mimea hapa nchini.
Aidha, Tanzania imeungana na nchi wanachama kuidhinisha Mpango wa nane wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia “Global Environmental Facility – GEF-8, utakaoitwa uhifadhi wa wanyamapori kwa maendeleo endelevu “Wildlife Conservation for Development Integrated Programme”;
Pia imeongoza nchi wanachama kupinga kuidhinishwa kwa azimio mahususi la uhifadhi wa misitu Resolution on CITES and forests kutokana na kutokushirikishwa ipasavyo kwa nchi wanachana kuhusu umuhimu wa azimio hilo katika uhifadhi.
Katika hatua nyingine imeungana na Afrika Kusini, Indonesia, Namibia, Mexico na Uingereza katika kupinga mabadiliko ya Kanuni za uendeshaji wa mkutano wa Nchi wanachama. Mabadiliko hayo yanalenga kuruhusu kujadiliwa na kuidhinishwa kwanza kwa ajenda zenye mashrti magumu ya kibiashara wakati wa Mkutano na kumpa mwenyeki mawanda mapana ya kufanya maamuzi,
Pia Tanzania imeungana na nchi wanachama kuidhinisha viashiria vya mpango Mkakati wa CITES yaani “CITES Strategic Vision 2021-2031”.
Ujumbe kutoka Tanzania katika mkutano huo unaotarajiwa kuhitimishwa leo Machi 11, 2022 unaongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Maurus Msuha huku wawakilishi wengine kutoka Tanzania wakiwa ni Dkt. Ernest Mjingo (Mkurugenzi Mkuu – TAWIRI) na Mabula Misungwi (Kamishna wa Uhifadhi – TAWA).
Wengine ni Dkt. Ismael Kimirei (Mkurugenzi – TAFIRI); Dkt. Chelestino Balama (TAFORI), Dkt. Dennis Ikanda (TAWIRI), Bw. Elisante Ombeni (Dawati la CITES – Idara ya Wanyamapori); Emmanuel Musamba (TAWA), Bw. Daniel Silima (TFS) na Meshack Meshilieki (TAWA).