Nchi wanachama wa Baraza la Michezo la Umoja wa Afrika Kanda ya IV zimeichagua Tanzania kuwa Makao Makuu ya Sekretarieti ya Baraza hilo linaloundwa na nchi 14.
Uteuzi huo umepatikana kupitia mkutano wa Baraza hilo uliofanyika jijini Arusha chini ya uongozi wa Mwenyekiti, Peter Ogwang ambaye ni Waziri anayeshughulikia masuala ya michezo nchini Uganda.
Tanzania imepitishwa na wajumbe kutoka nchi 14 zinazoshiriki mkutano huo ambazo ni Comoro, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Madagascar, Mauritius, Rwanda, Shelisheli, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Uganda na wenyeji Tanzania.
Akizungumza mara baada ya Tanzania kuchaguliwa, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Pindi Chana amewashukuru wajumbe hao akiwahakikishia kuwa Tanzania itakuwa tayari kusimamia, kuendeleza na kuhakikisha mipango na matarajio ya Baraza hilo yanafikiwa kwa mafanikio makubwa.
Pia amesema Sekta ya Michezo ni miongoni mwa tasnia zenye kujumuisha vijana wengi na hivyo kuthibitika kuwa chanzo imara cha ajira kwa vijana duniani kutokana na umuhimu wake kwa nchi na Jumuiya za Kimataifa ziliamua kutunga sheria, kanuni, taratibu na miongozo ili kuendeleza na kulinda vipaji vya wanamichezo katika nchi na jumuiya hizo.