Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika kudhibiti mfumuko wa bei wa Taifa ikilinganishwa na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha mwezi June , 2021.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii, Ruth Minja, Jijini Dodoma ambapo amesema kuwa mfumuko huo kwa hapa nchini kwa mwezi Juni umefikia asilimia 3.6 kutoka asilimia 3.3 mwezi Mei, Kenya 6.32 kutoka 5.87 ya mwezi Mei, 2021 na Uganda 2.0 kutoka 1.9 mwezi Mei, 2021 .
Akifafanua zaidi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuchukua hatua za kudhibi mfumuko wa bei ili kuwawezesha wananchi kuendelea kuchangia katika kukuza uchumi na shughuli nyingine za maendeleo.
Aidha baadhi ya bidhaa zilizoongezeka bei kwa mwezi June ni vitambaa vya nguo kwa asilimia 8.5, nguo za wanawake kwa asilimia6.3, viatu vya wanawake kwa asilimia 6.3, viatu vya wanaume kwa asilimia 6.2, kodi ya pango asilimia 4.9, vyakula kwenye migahawa asilimia 5.6 na gharama za malazi kwenye nyumba za kulala wageni kwa asilimia 5.7
Kwa upande wa bei za vyakula na vinywaji Baridi kwa mwaka ulioishia mwezi June, 2021 umepungua hadi asilimia 4.7 kutoka asilimia 4.9 kwa mwaka unaoishia mwezi Mei , 2021.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa sheria ya Takwimu Sura 351 na yenye mamlaka ya kutoa, kusimamia na kuratibu upatikanaji na usambazaji wa Takwimu rasmi.