Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza kuunga mkono tamko la Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) la kupinga vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Zimbabwe ilivyowekewa na mataifa ya Ulaya na Marekani.
Kwa mujibu wa SADC ni kuwa vikwazo hivyo vimerudisha nyuma uwezo wa Zimbabwe kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na vina athari kubwa zaidi kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa watu wa Zimbabwe hususan makundi maalum ya wanawake, watoto na wazee.
Vikwazo hivyo licha ya kuiathiri Zimbabwe, vina athari pia kwa Jumuiya za Kikanda na Kimataifa kwa kuwa vinainyima fursa nchi hiyo kushirikiana na Nchi Wanachama wa SADC na Umoja wa Afrika (AU) kibiashara na katika utekelezaji wa miradi ya ushirikiano ya Maendeleo.
Aidha, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaunga mkono hatua ya Umoja wa Mataifa (UN) kumwagiza Mjumbe wake, Profesa Alena Douhan kwenda nchini Zimbabwe kwa ajili ya kukutana na Rais wa Zimbabwe,. Emmerson Mnangagwa, Viongozi wa Taasisi za umma na Mashirika ya kiraia kwa lengo la kutathmini athari za vikwazo hivyo.
Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 17hadi 18 Agosti 2019 Jijini Dar es Salaam, uliidhinisha tarehe 25 Oktoba ya kila mwaka kuwa siku maalumu kwa nchi Wanachama wa SADC kupaza sauti kupitia majukwaa ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa kupinga vikwazo ambavyo mataifa ya Ulaya na Marekani yameendelea kuiwekea Jamhuri ya Zimbabwe kwa takribani miaka 18.