Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amewahakikishia kundi maalum la Wawekezaji na Watalii Mahiri Duniani zaidi ya 150 kutoka nchini Marekani na nchi nyingine lililowasili nchini Novemba 4, 2023 kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana nao kikamilifu katika jitihada za kukuza uchumi wa Tanzania kupitia sekta ya utalii
Akizungumza katika hafla iliyofanyika jijini Arusha, Kairuki amesema moja ya lengo kuu la hafla hiyo ni kuitangaza Tanzania kama kivutio cha utalii na pia soko la utalii la kuvutia na la uhakika kwa wageni wa Marekani.
“Serikali ya Tanzania inahimiza uwekezaji katika miundombinu na maendeleo ya masoko ya utalii na hii ni fursa nzuri kwa makampuni ya Marekani kuongeza mauzo na kupata maeneo ya kimkakati ya kukuza uwekezaji barani Afrika,” Kairuki amesisitiza.
Kuhusu ongezeko la Idadi ya watalii wanaotembelea nchini, Kairuki amesema mwaka jana ulikuwa mwaka wa rekodi kwa utalii nchini Tanzania, ambapo zaidi ya wageni milioni moja walikuja kufurahia maeneo ya ikolojia ambapo jumla watalii 100,600 walikuwa ni kutoka nchini Marekani.
Amesema ongezeko la idadi ya watalii linatokana na kuongezeka kwa utangazaji wa Utalii kupitia Filamu ya “Tanzania the Royal Tour” pamoja na matangazo ya Television ya CNN ambapo vivutio vya utalii vinaendelea kutangazwa duniani kote.
Aidha, Kairuki amesema Tanzania pia itakaribisha kikundi cha wachezaji 120 maarufu wa tenisi na wapenda tenisi kutoka Marekani ambao watakuwa kwenye McEnroe Luxury Safari Tour, na Mashindano ya Tenisi yatakayofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Desemba, 2023.