Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), limesema kwa sasa wametuma maombi ya usajili rasmi wa mbio za marathon za CRDB na NBC, ili zitambulike kimataifa na kuwavutia wanariadha wengi zaidi.
Makamu wa rais Shirikisho hilo, William Kallaghe, amesema wametuma maombi kwa Shirikisho la Riadha la Dunia kuomba kusajiliwa kwa mbio hizo ili ziungane na mbio za Kilimanjaro Marathon kuwa na leseni ya kimataifa.
“Kama tutafanikiwa, mbio hizi zitakuwa zikijulikana kimataifa na zitaitwa za kimataifa, faida yake kubwa, kwanza zitatambulika lakini pia zitawavuta wanariadha wengi duniani kuja kushiriki,” amesema Kallaghe.
Aidha, amesema kutambulika rasmi kimataifa kutazifanya mbio hizo kutumika kwa wanariadha kusaka viwango vya kushiriki mashindano makubwa zaidi yakiwamo ya dunia.
“Hapa nataka niwaeleweshe watu, si kila mbio ni marathon, watu siku hizi wanaandaa mbio za kilometa 10 wanaita marathon, mbio za marathon ni zile za kilometa 42, hizi ndio marathon na zile za nusu yake za kilometa 21 zile tunaziita nusu marathon,” amesema Kallaghe.
Kallaghe amesema kwa taasisi au watu wanaotaka kuanzisha mbio zozote ni vizuri kuwasiliana na RT kwa ajili ya kufuata taratibu na mbio hizo kutambulika.
“Kuna taratibu zake, riadha ni mchezo kama ilivyo michezo mingine ina kanuni na sheria zake, hivyo kwa taasisi inayotaka kuanzisha mbio zake ni lazima wawasiliane na sisi,” amesema Kallaghe. Amesema wanataka kuona Tanzania inakuwa na mbio zake za marathon zitakazokuwa zikitambulika duniani ambazo zitasaidia kuitangaza nchi na kuleta wageni wengi.