Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amesema Tanzania, Uganda na Kenya wako tayari kuandaa Fainali za MATAIFA YA Afrika ‘AFCON 2027’.
Dk Ndumaro ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania nchini Misri kushuhudia upigaji kura utakaotoa hatma ya nchi za Arika Mashariki kuandaa fainali hizo kesho Jumatano (Septemba 27).
Upigaji kura huo unatarajiwa kufarıyika ambapo nchi hizo tatu ziliwasilisha pamoja ombi kutaka kuwa mwenyeji wa michuano hiyo zikishindana na Senegal huku Nigeria na Botswana zikijitoa.
Akiwa Cairo, Dk Ndumbaro alikutana na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ Veron Mosengo Omba na kufanya mazungumzo katika Makao Makuu ya Shirikisho hilo yaliyopo Cairo.
Mazungumzo yao yalihudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Soka nchini Tanzania, Wallace Karia, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa, Neema Msitha na viongozi wengine wa TFF.
Pia Dk Ndumbaro aliongoza ujumbe wa Tanzania kutembelea Ubalozi Tanzania, Misri na kukutana na Balozi Dk Emanuel Nchimbi.
Alisema kupitia marais wa nchi hizo, wako tayari kuandaa mashindano hayo kwa kuwa zina mazingira mazuri ikiwamo miundo mbinu inayokidhi mashindano hayo kama viwanja, hoteli, usafiri na vivutio vya utalii.
Naye Balozi wa Tanzania nhini humo, Dk Emmanuel Nchimbi alisema atahakikisha anawashawishi mabalozi wa nchi mbalimbali kuunga mkono fursa hiyo adhimu kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania Wallace Karia alisema nchi hizo zinayo nafasi ya kushinda kwa kuwa hazijawahi kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ambapo amesema viwanja tisa vitatumika katika nchi hizo.