Tanzania imeibuka mshindi wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya duniani baada ya kufanikiwa kwa asilimia 90 kuwakamata wasafirishaji na wauzaji wakubwa wa mihadarati.
Hayo yamebainishwa na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya, James Kaji katika uzinduzi wa huduma za Methadone kwenye kituo cha Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo.
Amesema taarifa ya kimataifa ya mapambano ya dawa za kulevya inaonesha hadi mwaka jana, Tanzania ilikuwa imefanikiwa kupambana kwa asilimia 90.
Amebainisha kuwa kwa kipindi kifupi tangu kuundwa kwa mamlaka hiyo, jumla ya watuhumiwa 10,384 wakiwepo wauzaji na wasafirishaji wa dawa za kulevya wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.
Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigela amesema kutokana na mkoa huo kuwa lango la kupitisha dawa za kulevya na kushika nafasi ya pili kitaifa, kamati ya ulinzi na usalama imeelekeza nguvu zake kudhibiti uingizaji kupitia njia za panya za nchi kavu na majini.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Jonathan Budemo amesema kwa kipindi cha siku 10 jumla ya wateja 37 wamepokewa kituoni hapo na kupata huduma ya Methadone.
Mwakilishi wa shirika la Amref linalofadhili miradi ya huduma za Methadone, Florence Temu amesema kwa kushirikiana na wadau wengine wameweza kutoa milioni 20 kwaajili ya kujenga kituo cha muda cha kupokea waathirika wa dawa za kulevya katika hospitali hiyo na kuwapa matabibu.