TANZANIA imeongoza kwa ukuaji mzuri wa uchumi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na eneo zima la Mashariki mwa Afrika lenye nchi 13, katika kipindi chote cha janga la virusi vya corona.


Ripoti ya Uchumi wa Afrika ya 2020 ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imeonesha tathmini ya athari za virusi vya corona katika kanda tano za Bara la Afrika, ambapo Kanda ya Mashariki ndiyo iliyofanya vizuri zaidi kiuchumi.

Kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kipindi cha virusi vya corona, Tanzania imeongoza katika makadirio ya ukuaji wa uchumi kwa kuwa na wastani wa asilimia 5.2, ikifuatiwa na Rwanda (4.2), Uganda (2.5), Kenya (1.4), Sudan Kusini (-0.4) na Burundi (-5.2).

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mambo yaliyosababisha Afrika Mashariki na eneo zima la Mashariki mwa Afrika kufanya vizuri kiuchumi kuliko kanda zote barani Afrika ni pamoja na matumizi makubwa katika miundombinu, kupanda kwa mahitaji ya ndani, kuimarika kwa hali ya usalama, kuwapo kwa fursa mpya za uwekezaji na misamaha katika kuchochea ukuaji wa viwanda.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa Tanzania imefanikiwa kukuza kiuchumi wakati wa kipindi cha corona kutokana na hatua ilizochukuwa kukabiliana na maambukizi ya virusi hivyo bila kuathiri shughuli za kiuchumi na biashara, wakati nchi zilizochukua hatua kali, uchumi wake umeporomoka.

Sababu zilizotajwa za baadhi ya nchi kuporomoka kiuchumi ni kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo ziligeuzwa matumizi na kutumika katika kupambana na virusi hivyo.

Sababu nyingine ni kudorora kwa ukusanyaji wa mapato hasa kwa nchi zilizoweka na kutekeleza sheria ya kukaa ndani ‘lock down’ kama vile Kenya, Uganda, Sudan Kusini na Rwanda.

Ripoti hiyo ilisema ukusanyaji wa mapato katika nchi hizo, ulikuwa mdogo kwa kuwa biashara nyingi zilifungwa kwa ajili ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania ndio taifa la kwanza kufungua milango ya kiuchumi na kutoweka sheria ya ‘lock down’, hali inayotajwa na ripoti hiyo kuwa yenye manufaa makubwa kwa uchumi wake na kanda nzima ya Afrika Mashariki.


Wamiliki wa 'pool table' waagizwa kujisajili
TCRA, NEC wawafunda watoa huduma ya habari mitandaoni

Comments

comments