Kampuni maarufu ya Uholanzi, LIMAX B.V. (LimaxGroup) imedhamiria kuwekeza kwenye Sekta ya Uyoga nchini Tanzania kwa kujenga kiwanda cha kusindika na kukausha uyoga Mkoani Iringa kwa thamani ya Euro milioni 2.1 ambazo ni sawa na Shilingi Bilioni 5.5 za Tanzania.
Hayo yameelezwa kufuatia Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Irene Kasyanju kutembelea kampuni hiyo tarehe 26 Agosti 2021 na kufanya
mazungumzo na Mkurugenzi na Mmiliki wa kampuni hiyo, Tom VanWalsem.
Balozi Kasyanju ameeleza kuwa uwekezaji huo utakapokamilika, Tanzania itafaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na mtiririko wa biashara ya uyoga kukua kwa kasi duniani ambapo kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), biashara hiyo inakadiriwa kuongezeka hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 62.2 ifikapo mwaka 2023 kutoka Dola za Marekani bilioni 42.4 mwaka 2018.
“Tanzania ni nchi yenye maeneo makubwa ya misitu yenye
aina anuwai ya uyoga wa porini kwa ajili ya kula, na jamii zimekuwa zinategemea maarifa asilia kukusanya uyoga huo kwa matumizi na kuuza katika masoko ya ndani tu. Ni wakati muafaka sasa kufanya kazi pamoja kukuza ukuaji wa sekta hii kibiashara,” Amesema Balozi Kasyanju.
Aidha LIMAX Group itatoa mafunzo ya kuhifadhi na kuvuna uyoga wa
porini kwa madhumuni ya biashara na kulinda mazingira pia.
Hata hivyo ujenzi wa kiwanda hicho mkoani Iringa kutawawezesha wakulima kuuza uyoga wanaozalisha moja kwa moja kiwandani, lakini pia kuongeza ajira kwa Watanzania na kukuza mnyororo wa thamani
wa kilimo cha uyoga nchini.