Timu ya taifa ya soka la ufukweni ya Tanzania imefuzu kucheza fainali za Afrika zitakazofanyika nchini Misri, kufuatia kujitoa kwa waliokuwa wapinzani wao Afrika Kusini.
Mchezo kati ya wawili hao ulikua umepangwa kuchezwa Septemba 09 jijini Dar es salaam, kabla ya kurudiana nchini Afrika kusini majuma mawili baadae.
Tayari timu ya taifa ya Tanzania ya Soka la Ufukweni ilikuwa kambini kujiandaa na mchezo huo, ambao ulipangwa kuchezwa kwenye fukwe za Coco.
Taarifa iliyotumwa na afisa habari na mawasiliano wa Shirikisho la soka nchini TFF Cliford Mario Ndimbo, imeeleza kuwa, timu ya Tanzania imefuzu kucheza fainali za Afrika baada ya mpinzani wake Afrika Kusini kuwasilisha barua ya kujiondoa katika mashindano.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa, shirikisho la soka barani Afrika CAF tayari limewajulisha TFF juu ya kufuzu kucheza fainali hizo za Afrika zitakaofanyika Misri mwaka huu kuanzia Desemba 9-Desemba 14,2018 na kushirikisha nchi Nane.