Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini msaada wa shilingi Bilioni 490 kutoka Umoja wa Ulaya ambapo msaada huo ni wa bajeti kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka wa bajeti wa 2017/18 na hauna masharti yeyote.
Msaada huo umesainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James kwa niaba ya Serikali na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Roeland van de Geer kwa niaba ya Umoja wa Ulaya.
Umoja wa Ulaya umetoa msaada huo kutokana na kuvutiwa na juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika maeneo mbalimbali ikiwemo kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu huyo mara baada ya kusaini msaada huo kwa niaba ya Serikali ambapo pia ameeleza kuwa Umoja wa Ulaya wametuihakikishia Serikali ya Tanzania kuendelea kuisaidia katika masuala ya misaada ya kibajeti pamoja na kuwa bega kwa bega katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
Amesema mpango wa pili wa maendeleo wa Taifa wa Bajeti ya mwaka 2017/18 pia utapewa msaada na umoja huo kwani wameuona mpango huo una tija na kuweka mkazo katika viwanda na kilimo.
Naye Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Roeland Van de Geer amesema msaada huo uliokwisha kusainiwa utaiwezesha Wizara ya Fedha na Mipango katika ukusanyaji wa mapato, kuboresha uwajibikaji na utumiaji mzuri wa mali za Serikali, na Umoja wa Ulaya unasapoti azma ya viwanda ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Amesema wameliangalia zaidi suala la utawala kama eneo kuu katika mpango wa ushirikiano na Tanzania na vilevile wanatazamia maendeleo zaidi katika maeneo ya kilimo, ujenzi wa barabara za vijijini na nishati.
“Mkataba ambao tumeusaini utaiwezesha Wizara ya Fedha na Mipango katika ukusanyaji wa mapato, zitaboresha uwajibikaji na utumiaji mzuri wa mali za Serikali, na Umoja wa Ulaya unasapoti azma ya viwanda ya Serikali ya Awamu ya Tano,”Aliongeza Roeland Van de Geer.
Aidha, amesema kuwa ushirikiano utaendelea kuimarika zaidi katika kipindi hiki ambacho mageuzi ya sera yanahitajika kwani uhusiano uliopo kati ya Tanzia na Umoja wa Ulaya ni mpana sana.