Serikali ya Tanzania imetoa msaada wa dawa, chakula na vifaa vya kujihifadhi kwa nchi ya Msumbiji, Malawi na Zimbabwe kufuatia athari za kimbunga cha Idai kilichosababisha maafa makubwa katika nchi hizo ikiwa pamoja na vifo vya watu wengi huku wengine wakikosa mahali pa kuishi.

Msaada huo umekabidhiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kwa mabalozi wa nchi hizo katika uwanja wa ndege wa Taifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere leo.

Wakati wa makabidhiano ya msaada huo Prof. Kabudi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais, John Pombe Magufuli ameagiza misaada hiyo itolewe pamoja na salamu za pole kwa nchi hizo zilizokumbwa na maafa hayo.

Aidha katika misaada hiyo yametolewa malori 7 yenye shehena ya tani 200 za mahindi yanayondoka leo kutoka Mbeya kwenda nchini Malawi ambako taarifa zinaonyesha kuwa watu 122 wamepoteza maisha huku watu 1000 wamekosa mahali pa kuishi.

Ambapo pia tani 7 za mchele na vifaa vya kujihifadhia leo vitaondoka kutoka Dar kwenda Msumbiji kwa kutumia ndege ya kijeshi ambako watu 221 wanasemekana kupoteza maisha.

Upande wa Afya, Ummy Mwalimu amesema wametoa msaada wa tani 24 za dawa ambapo kila nchi itapatiwa tani 8 za dawa za kuzuia maambukizi ya magonjwa, dawa za maumivu ya tumbo pamoja na dawa za maumivu.

Aidha balozi wa Malawi, Glad Chembe Munthali, Balozi wa Msumbiji, Monica Mussa na balozi wa Zimbabwe hapa nchini, Martin Tavenyika wamemshukuru rais Magufuli kwa msaada huo wa haraka uliodhihirisha undugu na ujirani mwema baina ya nchi za Afrika Mashariki.

 

 

 

Rais Magufuli afanya uteuzi mwingine
Prof. Lipumba azungumza na wapemba, 'Msifuate upepo''