Serikali ya Tanzania imewasilisha miradi minane yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.334 katika Mkutano wa Nane wa Kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaohusu ushirikiano wa Maendeleo baina ya Japan na Afrika (TICAD8), uliomalizika jijini Tunis, Tunisia.
Hayo yamenainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hii leo Agosti 29, 2022 jijini Tunis, na kusema uwasilishaji huo umefanywa mara baada ya kupata fursa ya kuwaeleza washiriki wa mkutano huo na nchi ya Japan, juu ya utekelezaji wa miradi kwa Tanzania Bara na Zanzibar kwa niaba ya Rais Samia.
Amesema, “Kupitia mikutano ya TICAD, sisi tumenufaika na ujenzi wa daraja la Mfugale, mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi II, na sasa tumeomba watukamilishie miradi mitatu ya barabara ya Arusha-Holili, Bandari ya Kigoma na mradi wa maji wa Zanzibar.”
Miradi hiyo mitatu iliyoombewa fedha, inahitaji dola milioni 343.8 ambapo kati ya hizo dola milioni 221 ni kwa ajili ya mradi wa barabara ya Arusha-Holili, dola milioni 98.7 (mradi wa kuboresha miundombinu ya usambazaji wa maji Zanzibar) na dola milioni 24.1 kwa ajili ya Bandari ya Kigoma katika ziwa Tanganyika.
Aidha, Waziri Mkuu pia amesema amezungumzia sekta ya Kilomo katika mkutano huo, ambapo ameomba kupewa kipaumbele ili Tanzania iweze kuongeza wigo wa kilimo na kujihakikishia uhakika wa chakula kingi cha biashara na akiba.
Kwa upande wake Rais wa JICA, Dkt. Akihiko Tanaka amemuahidi Waziri Mkuu kuwa, wafanyakazi wa kujitolea waliokuwa wakifanya kazi Tanzania na kulazimika kurudi Japan kwa sababu ya UVIKO-19 wataanza kurejea hivi karibuni ili waendelee za utoaji wa huduma.
Miradi iliyowasilishwa katika mkutano huo ni pamoja na ukarabati wa barabara ya Morogoro-Dodoma kwa kiwango cha lami, mradi wa umwagiliaji katika bonde la Ziwa Victoria, na mradi wa kusambaza maji Lugoda, Mufindi – Iringa.
Mingine ni ile ya kujenga uwezo wa kituo cha utafiti cha ufugaji wa samaki Dar es Salaam, bandari ya kisasa ya uvuvi, kuanzisha maabara ya kuthibitisha ubora kwenye sekta ya uvuvi na ukarabati wa bandari ya uvuvi ya Wete na ujenzi wa njia ya umeme ya Somanga-Fungu-Mkuranga.