Mapema leo alfajiri, Watanzania walipokea taarifa za kusikitisha za kifo cha mwanasiasa mpambanaji, Mchungaji Christopher Mtikila.

Taarifa za kifo cha Chungaji Mtikila zilithibitishwa na Kamanda wa polisi Mkoa wa Pwani, Jaffar Mohamed. Kwa mujibu wa taarifa za jeshi la polisi, Mchungaji Mtikila alifariki baada ya gari dogo alilokuwa akisafiri nalo kutoka Morogoro kuelekea Dar es Salaam kupata ajali katika Kijiji cha Msolwa, Chalinze, Pwani, alipokuwa akitokea Morogoro kuelekea Dar es Salaam.

Ndani ya gari hilo, Mchungaji Mtikila alikuwa na watu wengine watatu ambao walinusurika na wanaripotiwa kupata majeraha kadhaa.

Katika hali ya kusikitisha, pamoja na mambo mengine, Mchungaji Mtikila alikuwa amebeba ndoto kubwa ya kubadilisha hali ya uchaguzi mkuu nchini kwa kuwa na mgombea binafsi wa nafasi ya urais.

Mchungaji Mtikila alifungua kesi katika mahakama za juu za Tanzania na kufanikiwa kushinda japo mahakama ilirudisha suala hilo kujadiliwa ndani ya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na mazingira ya sasa ya nchi yetu.

Ingawa baadhi walimuona kama mtu anaeibua vitu ambavyo havikutarajiwa na wengi kuwa sehemu ya mashtaka, kesi za Mchungaji Mtikila dhidi ya serikali mara kadhaa zimekuwa za kushangaza lakini zimekuwa zikizaa matunda na yeye kupewa ushindi kwa asilimia kubwa ya kesi hizo.

Upekee wa kesi za Mchungaji Mtikila zimekuwa zikikidhi vigezo vya kisheria na baadhi kutumika kama mfano wa kesi zinazofundishiwa vyuo vikuu(case laws), ambazo pia ni vyanzo vya sheria (precedent). Hivyo, kesi za Mchungaji Mtikila zimekuwa sehemu ya chanzo sheria nyingine.

Hivi karibuni, Mchungaji Mtikila alikuwa anaendelea na ndoto yake ya kugombea na kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini kwa bahati mbaya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilikataa kumpitisha kutokana na kile ilichodai fomu zake kutokidhi vigezo na taratibu.

Hata hivyo, Mchungaji Mtikila aliamini kuwa NEC walimuonea hivyo akapeleka malalamiko yake mahakamani na alikuwa anasubiri mahakama kutoa maamuzi hivi karibuni kabla ya Oktoba 25.

Wiki iliyopita, Mchungaji Mtikila alionekana kwenye vituo kadhaa vya runinga nchini akieleza kuwa anaamini atashinda na kuendelea kuwa kati ya wagombea urais wa mwaka huu na kwamba anaamini angeweza kuwa rais wa nchi hii, ndoto ambayo imekatashishwa baada ya ajali ya gari kuchukua uhai wake.

Tunaamini harakati za Mchungaji Mtikila zimeacha mbegu kwenye muenendo wa kisheria nchini na katika siasa za nchi hii hivyo matunda yake yataendelea kuonekana.

Dar24 inawapa pole familia ya Mchungaji Mtikila pamoja na watanzania kwa ujumla. Apumzike kwa amani.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Mpango Wa Dk. Slaa Dhidi La Lowassa Na Ukawa Sasa Hadharani
Amshtaki Mbunge Wa Chadema Kwa Magufuli Kwa Tuhuma Za Kubakwa na Viongozi wa CCM