Uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) umetangaza taarifa ya vifo vya watumishi wake watano kutokana na ajali ya treni ya uokoaji kugongana na kiberenge namba HDT – 3 katika eneo lililopo kati ya stesheni ya Mwakinyumbi na Gendagenda tarehe 22 Machi 2020.
Imeelezwa kuwa ajali hiyo imehusisha watumishi sita wa TRC ambapo watumishi wanne walifariki eneo la ajali na majeruhi wawili walifikishwa katika hospitali ya wilaya ya Magunga iliyopo Korogwe mkoani Tanga.
Wakati majuruhi wakiwa wanaendelea kupatiwa matibabu, ilipofika saa tano usiku majeruhi mmoja alifariki na kufikia jumla ya vifo vya watumishi watano katika ajali hiyo.
Watumishi waliopoteza maisha ni, Meneja usafirishaji kanda ya Tanga, Ramadhani Gumbo, Meneja ukarabati wa mabehewa ya abiria kanda ya Dar es salaam Eng. Fabiola Moshi, Meneja msaidizi usafirishaji kanda ya Dar es salaam Joseph Komba, Mtaalamu wa usalama wa reli Philibert Kajuna na dereva wa kiberenge George Urio.
Mpaka sasa majeruhi mmoja ambaye ni muongoza treni Elizabeth Bona anaendelea na matibabu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uchunguzi wa kujumuisha ili kubaini chanzo cha ajali hiyo bado unaendelea kwa kushirikiana na taasisi nyingine zenye mamlaka hiyo.