Kampuni ya TAQA ARABIA ya Misri imeahidi kujenga vituo 12 vya kusambaza gesi asilia nchini kuanzia kipindi cha mwaka 2023, pamoja na kujenga uwezo wa vijana kuhusu teknolojia ya gesi katika vyombo vya usafiri.
Hayo yamebainishwa hii leo Mei 11, 2023 jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama wakati akifungua Warsha ya Kujadili Matokeo ya Mkutano wa 27 na Maandalizi ya Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.
Amesema, “Mtakumbuka katika Mkutano wa COP 27 Tanzania ilikuwa na banda lake ambalo uwepo wake umetoa fursa kubwa kwa Tanzania kujulikana na kupatikana kirahisi wakati wa mikutano ikiendelea na kufanya majadiliano na kutoa ufafanuzi kuhusu fursa za uwekezaji na ushirikiano na vipaumbele vya nchi kuhusu hifadhi na usimamizi wa mazingira.“
Mkama ameongeza kuwa, Shirika la The Nature Conservancy (TNC) lipo tayari kuisaidia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuanza biashara ya kuuza Hatifungani za Bluu (Blue Bond).
Tanzania, ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika na programu ya uchumi wa bluu na kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika bara la Afrika inayofadhiliwa na Benki ya Dunia ambapo Serikali ya Norway imeahidi kuendeleza msada katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi.