Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania – TARI, imedhamiria kuondoa changamoto ya zao la ngano nchini, kutokana na mahitaji ya ngano yalivyo kwa sasa kwa mwaka, kuwa ni tani 1,000,000 na uzalishaji uliopo ni tani 100,000 sawa na upungufu wa tani 900,000.
Akiongea katika maonesho ya wakulima yanayoendelea mkoani Mbeya, Mratibu wa zao la ngano Kitaifa – TARI kituo cha Selian Arusha, Ismail Ngolida amesema hatua hiyo itasaidia kuondoa mzigo mkubwa na kutumia fedha nyingi za kigeni kuiagiza kutoka nje.
Amesema, “ifikapo mwaka 2030 kunahitajika kuwe na uzalishaji unaofikia tani 2500 za mbegu za awali ambazo hizi mbegu za awali zitaweza kuzalisha tani 50,000 za mbegu zilizothibitishwa ubora, Mbegu hizi sasa zinaweza kupandwa eneo linalozidi hekta 400,000 ambazo zinaweza kutupatia hayo mahitaji ya ngano.”
Hata hivyo, Ngolida ameongeza kuwa moja ya mikakati ambayo Serikali ilimejiwekea ni kuzalisha mbegu za kutosha pamoja na kuongeza maeneo ya uzalishaji wa ngano, ili ifikapo mwaka 2030 nchi iwe imejitosheleza kwa uzalishaji wa zao hilo muhimu nchini.