Baada ya kumalizana na Geita Gold, kiungo Tariq Simba ameomba ushirikiano kutoka kwa wachezaji, viongozi na Benchi la Ufundi la timu hiyo.

Tayari uongozi wa Geita Gold kupitia kwa Mtendaji Mkuu, Simon Shija umetangaza kumalizana na mchezaji huyo ambaye anamudu kucheza nafasi ya kiungo na beki wa kushoto.

Simba ambaye msimu uliopita aliichezea Polisi Tanzania amesema, anashukuru kwa kupewa nafasi nyingine ya kuonyesha uwezo wake lakini akaomba ushirikiano kutoka kwa wachezaji Benchi la Ufundi pamoja na viongozi wa timu hiyo.

“Nashukuru kwa kupata nafasi nyingine ya kuonesha uwezo wangu, nitaipambania timu yangu kuhakikisha inafanya vizuri.”

Mchezaji huyo wa zamani wa Biashara, alitumia nafasi hiyo kuwaaga Polisi Tanzania ambayo aliitumikia kwa misimu miwili 2020-2021na 2022-2023.

“Ilikuwa sehemu sahihi kwangu, nimepata ushirikiano wa kila aina kutoka kwa wachezaji wenzangu, viongozi na Benchi la Ufundi, nitumie nafasi hii kuwaaga, kwaherini mtabaki kuwa ndugu zangu,” amesema Simba ambaye amewahi pia kuichezea Tunduru Korosho.

Tanzania inapambana na vita ya uchumi - Chongolo
Yusuph Kagoma: Ligi Kuu itakuwa ngumu sana