Chama cha watu wenye Ualbino Tanzania (TAS), Mkoa wa Morogoro kimeendelea kutekeleza programu ya kuelimisha wanafunzi juu ya haki za watu wenye ualbino, kama njia mojawapo ya kulinda kundi hilo na kuimarisha utangamano nao kwenye jamii.
Akifafanua kuhusu zoezi hilo, Mwezeshaji wa programu hiyo kutoka TAS, Julia Kayombo amesema wamewaeleza wanafunzi malengo ya chama cha watu wenye ualbino Tanzania na kugusia changamoto anazokutana nazo mtu mwenye ualbino na jinsi ya kuzitatua.
Amesema, “Tumeelimisha jinsi ya wao kutoa elimu kwa Jamii zao jinsi ya kuwalinda watu wenye ualbino, kutowatenga na zaidi na tumeona tutoe elimu kwa watoto walio katika shule za msingi na sekondari.”
Bi. Kayombo ameongeza kuwa, kwa kutumia rika hilo kuwapa elimu inawapa imani kuwa rika hilo litaenda kuwaelimisha na wengine na kuleta uelewa kwa Jamii ili kuepusha masuala ya unyanyapaa unaosababisha kutojiamini kwa wenzao.”
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi, waliopatiwa elimu ya Ualbino wanasema wameupokea vyema ujumbe huo na kuahidi kuufanyia kazi katika maisha yao ya kila siku ili kuleta ufahamu kwa walio wengi.
Katika tukio la hivi karibuni, TAS mkoani Morogoro ilitembelea shule ya msingi ya Kilakala ya Manispaa ya Morogoro ambako walizungumza na wanafunzi wa darasa la 6 na la 7 jinsi ya kuishi na watoto wenye ulemavu wa ngozi katika jamii.