Eva Godwin – Dodoma.
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania – TASAC, limeanza majukumu ya udhibiti wa huduma za usimamizi wa ulinzi na usalama na kuzuia uchafuzi wa mazingira utokanao na shughuli za usafiri majini.
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dodoma hii leo Julai 27, 2023, Mkurugenzi wa TASAC Kaimu Abdi Mkeyenge, amesema majukumu hayo awali yalikuwa yakifanyika chini ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini – SUMATRA.
Amesema, pamoja na kusimamia Ulinzi na Usalama wa Usafiri Majini na Kuzuia Uchafuzi wa Mazingira utokanao na shughuli za usafiri majini, TASAC pia itasimamia na Kudhibiti Watoa Huduma za Usafiri na Usafirishaji kwa njia ya maji nchini.
“Jukumu la udhibiti kwa Watoa Huduma za Usafiri na Usafirishaji kwa njia ya maji nchini linahusu Watoa Huduma za Bandari, Bandari Kavu, Upimaji wa Uzito wa Makasha, Uwakala wa Melina Uwakala wa Forodha,” amesema Mkeyenge.
Hata hivyo, amesema zoezi la urasimishaji wa bandari bubu 13 Tanzania bara zilizowasilishwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari – TPA, zilikaguliwa na kufanyiwa tathmini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania – TRA na Baraza la Usimamizi wa Mazingira – NEMC.
Amesema, “Bandari bubu 10 zilionekana kukidhi vigezo na kupendekezwa kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) kwa ajili ya kurasimishwa kwa mujibu wa sheria na waendeshaji wa zilizokuwa bandari bubu binafsi tano za Mwanza ambazo ni miongoni mwa zilizokuwa bandari bubu 20.
Aidha, Mkurugenzi huyo amesema Bandari hizo zilizorasimishwa kupitia Tangazo la Serikali zilipewa leseni za uendeshaji huku TPA wakielekezwa kusimamia kwa karibu bandari 15, zilizobakia.