Kamati ya Utendaji ya Chama na Waandishi wa Habari za Michezo ‘TASWA’ imefikia uamuzi wa kurejesha Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa kila mwezi iliyokuwa ikitolewa na chama hicho TASWA miaka ya nyuma.

Maamuzi hayo yamefikiwa baada ya kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Aprili 30, 2023.

Taarifa ya TASWA iliyosainiwa na Katibu Mkuu Alfred Lucas imeeleza, Tuzo hiyo itakayoanza kushindaniwa mwezi Julai, 2023 na mshindi wake kupatikana Agosti 2023, itahusisha wanamichezo wote wanaocheza Tanzania, ambao michezo yao inatambuliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na wale ambao ni Watanzania lakini wanacheza nje ya Tanzania.

Baada ya kupatikana mshindi wa kila mwezi kwa mwaka mzima 2023/2024, TASWA itaandaa sherehe za Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Tanzania kwa mwaka, ambaye mshindi wa jumla atatoka miongoni mwa washindi wa mwezi.

Pia katika sherehe hizo TASWA itazawadia wanamichezo wengine waliofanya vizuri kwa michezo yote inayotambuliwa na BMT, ambao kwa mwaka 2023/2024 michezo yao itakuwa imefanya mashindano kitaifa au kimataifa na kuonekana wanastahili tuzo.

Jukumu la uratibu wa tuzo hiyo ya kila mwezi pamoja na ile ya mwaka litasimamiwa na Kamati ya Tuzo za TASWA, ambayo tayari imeundwa na itatangazwa hivi karibuni.

Pobga apata majanga Juventus
Mayele: Tutapambana hadi kieleweke