Kocha mpya wa Inter Miami, Gerardo ‘Tata’ Martino amesisitiza kwamba yeye na wachezaji wajao waliosajiliwa Lionel Messi na Sergio Busquets hawajenda huko kama likizo.
Martino alitangazwa kuwa bosi mpya wa Miami Jumatano, ambapo anatazamiwa kuungana tena na Messi na Busquets, ambao awali aliwafundisha FC Barcelona.
“Tulipozungumza na Leo, jana (juzi) nilizungumza na Sergio, tulizungumza kuhusu kufika ili kuwa na mafanikio, kushindana na kushindana vyema,” alisema Martino wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari.
Hii inatokea kwetu hata kwa viwango vya kibinafsi, wakati mwingine watu wanaweza kudhani kuja Marekani ni kama likizo….. wanasoka ambao watakuja hapa ni kwa ajili ya kushindana.”
Mapema mwezi huu, Messi alitangaza uamuzi wake wa kujiunga na Miami, ambayo ilifuatiwa na habari za wiki jana kwamba kiungo Busquets pia atajiunga na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya soka ya Marekani, MLS.
Martino aliwafundisha wachezaji wote wawili wakati wa uongozi wake kule Barcelona kutoka mwaka 2013 hadi 2014, pamoja na Messi katika ngazi ya kimataifa na Argentina kuanzia mwaka 2014 hadi 2016.
Martino ambaye anarejea MLS baada ya kuiongoza Atlanta United katika misimu ya 2017 na 2018, alisema mazungumzo na Miami yalianza kabla ya mikataba ya wachezaji wote wawili.
“Nilianza mazungumzo kabla ya kusajiliwa kwa Messi na Busquets,” alisema kocha huyo raia wa Argentina.
Pamoja na kuwasili kwa nyota huyo wa kimataifa na bingwa wa Kombe la Dunia la 2022 kwa MLS, Martino alisema Messi mwenye umri wa miaka 36 anaweza kusaidia zaidi kuhamasisha ukuaji wa soka nchini Marekani.
“Nimesoma kwamba wachezaji wa NFL na NBA wanazungumza juu ya hali hii, ambayo inaonekana kuwa nadra sana,” amesema.
“Ninaamini kwamba MLS ina mageuzi ya mara kwa mara na mifano ni wachezaji wa soka wa Marekani ambao wanacheza Ulaya, na katika timu nzuri sana za Ulaya. Tayari kuna mchakato ambao umeanza.”