Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendeleza kilimo cha mazao ya chakula na biashara ili kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika wa usalama wa chakula na ziada kuuza nje.
Ameyasema hayo leo Septemba 16, 2021 baada ya kukagua shamba la michikichi la kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) 821 KJ Bulombora akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Kigoma.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Serikali imeamua kulipa kipaumbele zao hilo ili kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini, ambapo Serikali inatumia zaidi ya sh. bilioni 400 kwa mwaka kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi, hivyo ufufuaji wa zao hilo utaliwezesha Taifa kuzalisha mafuta ya kutosha.
Aidha amewasisitiza wakuu wa Wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Kigoma kuratibu vizuri kilimo hicho ikiwa ni pamoja na kuwa na kanzidata itakayoonesha idadi ya wakulima, ukubwa wa mashamba yao na maeneo wanayolima ili kurahisisha utoaji wa huduma.
Naye Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele amesema katika kambi hiyo wamepanga kupanda ekari 2,000 za michikichi kwa awamu, ambapo mwaka jana walipanda ekari 500 na mwaka huu wanatarajia kupanda eneo jingine la ukubwa wa ekari 500.