Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima amesema zaidi ya mapadri 25, watawa zaidi ya 60 na wazee wawili wa Baraza la Walei wamefariki dunia ndani ya miezi miwili kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo changamoto ya upumuaji.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa Padri Kitima leo katika Mkutano na waandishi wa habari, viongozi wa kiroho wamefariki dunia katika maeneo mbalimbali kati ya Desemba, 2020 hadi Februari 2021 .
Padri Kitima amewataka waumini wa kanisa hilo kuendelea kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo yaliyotolewa na Serikali.
“Naomba muendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa kwa kufuata maelekezo ya Wizara ya Afya, Mapadri wanakufa na Masista wanakufa lakini ndani ya hii miezi miwili imetushtua sana hasa ukizingatia Serikali imeimarisha mifumo bora ya afya,” amesema Padri Kitima.
Amesema kuwa Rais wa TEC, Askofu Gervas Nyaisonga amesambaza mwongozo kwa Maaskofu wa Majimbo mbalimbali kuhusu hatua za kuchukua kujikinga na maambukizi ya corona.