Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania -TAWA, kuhakikisha wanamaliza tatizo la Wanyama wakiwemo Tembo kuvamia Makazi na Mashamba ya Wananchi Wilayani Manyoni.
Serukamba ameyasema hayo katika Vijiji vya Mpapa, Simbanguru na Nkonko wakati akisikiliza Kero za Wananchi hao huku Wananchi wa maeneo hayo wakisema kwa kipindi kirefu Wanyama hao wamekuwa wakivamia Makazi na kula nafaka ikiwemo mahindi aidha kwa kipindi cha Kilimo, Tembo uharibu Mashamba na wakati mwingine kusababisha majeruhi na vifo.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi – Kanda ya Kati -TAWA, Herman Nicholaus Nyanda – amesema Serikali kupitia TAWA wameendelea Kufanya jitihada za kuwafukuza Tembo pindi wanapopata Taarifa za uvamizi wa Wanyama katika Makazi na Mashamba ya Wananchi.
Amesema Jeshi la Uhifadhi Kanda ya Kati wametoa na inaendelea kutoa Elimu kwa Wananchi juu ya kujilinda na kuzuia Tembo kutofika katika maeneo ya Mashamba na Makazi ikiwemo kulima na kutumia pilipili, oili chafu na kuchimba mifereji ili kupunguza athari za Wanyamapori hao.
Mkuu huyo wa Mkoa ameendelea na ziara ya kijiji kwa Kijiji ambapo katika maeneo hayo amekuwa akipokea na kutatua Kero za Wananchi, Kufikisha Salamu za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan na kukagua miradi ya Maendeleo Katika Vijiji vyote vya Mkoa wa Singida.