Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa jengo la ofisi ya Jaji Kanda ya Shinyanga ili aweze kuhamia na kuanza kuitumia.
Kasekenya, ameyasema hayo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi unaosimamiwa na TBA wa jengo hilo pamoja na lile la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, huku akihimiza ujenzi wa majengo bora yatakayodumu kwa muda mrefu.
Awali, akitoa taarifa ya miradi hiyo, Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Nestory Nanguka amesema mpaka sasa ujenzi wa jengo la ofisi ya Jaji Kanda ya Shinyanga umefikia asilimia 85 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu wa 2022 huku ujenzi wa jengo la Mkuu wa Wilaya ya Kishapu ukifikia asilimia 65.
Naibu Waziri Kasekenya, yupo mkoani Shinyanga kwa ziara ya kikazi, akikagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na kusimamiwa na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.