Mshike Mshike wa Ligi ya Championship utaanza rasmi Septemba 9, tofauti na ilivyopangwa awali kuanza kesho Jumamosi (Septemba 2).
Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi (TPLB), Karim Boimanda amethibitisha mabadiliko hayo kwa kusema kuwa, wameamua kufanya mabadiliko hayo kwa lengo nzuri tu kuzipa timu shiriki muda mzuri wa kujiandaa.
“Ushindani tunaouona huku Ligi Kuu ndio ambao tunataka kuuona pia hata Championship japo kila mmoja wetu anatambua ubora uliopo, tunataka kuona timu zote zikijiandaa vizuri zaidi ya msimu uliopita,” amesema.
Boimanda ameongeza muda wowote kuanzia sasa ratiba ya ligi hiyo itatoka ili kila timu kujua inaanzia wapi.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Mbuni, Leonard Budeba amesema licha ya ligi hiyo kutoanza ila ni wazi msimu huu utakuwa ngumu kutokana na tỉmu zote zinazoshiriki kusajili wachezaji wenye hadhi ya Ligi Kuu.
Timu 16 zinazoshiri ligi hiyo ni; Pamba Jiji, Copco (Mwanza), Mbeya City, Mbeya Kwanza, KenGold (Mbeya), TMA, Mbuni (Arusha), Cosmo, Transit Camp, Pan Africans na Green Warriors za Dar es Salaam.
Nyingine ni Fountain Gate (Morogoro), Biashara United (Mara), Polisi Tanzania (Moshi), Ruvu Shooting (Tringa) na Stand United ya Shinyanga.