Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesema kuwa halijabaini kuwepo kwa sukari isiyofaa iliyoingizwa nchini baada ya kufanya ukaguzi kwenye vyanzo mbalimbali.
Mkurugenzi wa TBS wa idara ya ubora, Tumaini Mtitu amesema kuwa wanafanya kila liwezekanalo kudhibiti sukari isiyofaa kwa matumizi ya binadamu kuingia nchini, na kwamba hadi sasa hawajabaini kuwepo kwa tatizo hilo.
“Tunafanya ukaguzi wetu wa kawaida. Hadi wakati huu bado hatujabaini kuwepo kwa tishio la aina yoyote kuhusu usalama wa sukari inayotumika ndani ya nchi,” alisema Mtitu.
Kwa upande wake Msemaji wa Mamlaka ya Dawa na Chakula (TFDA), Gaudencia Simwanza alieleza kuwa Mamlaka hiyo pia haijabaini uwepo wa sukari isiyofaa na kwamba sukari inayoingia nchini kupitia njia halali hukaguliwa na kuruhusiwa kuingia sokoni pale tu inapokidhi viwango.
“Sina taarifa za kuwepo kwa sukari ambayo haifai kwa matumizi ya binadamu. Sukari inayongia nchini huruhusiwa kuingia sokoni pale tu inapokidhi viwango vya ubora,” alisema Simwanza.
Maelezo hayo ya Mamlaka hizo mbili zinazoshughulikia ubora wa chakula kwa ujumla, yamekuja kufuatia malalamiko ya wafanyabiashara wenye leseni za kuingiza sukari nchini kudai kuwa wameshindwa kuuza kiasi kikubwa cha mzigo wao kutokana na kuingia kinyamela kwa sukari kutoka nje.
Wakizungumza jana jijini Dar es Salaam kwenye kikao kilichohudhuriwa na waandishi wa habari, wafanyabiashara hao walidai kuwa hadi sasa wana zaidi ya tani 80,000 za sukari waliyoingiza nchini ambayo imekosa soko kutokana na kushindwa kushindana na bei ya sukari iliyoingizwa kinyamela.
Walifafanua kuwa wanaoingiza sukari kinyamela hukwepa kodi na hivyo kupunguza bei.
Kagera Sugar Ltd, Kilombero Sugar, Mtibwa Sugar Estates Ltd na TPC Ltd wamesema kuwa wamefanya utafiti wao na kubaini uwepo wa wafanyabiashara wanaoingiza kinyamela sukari kutoka nje ya nchi na kuziweka kwenye vifungashio vya sukari ya ndani ili kukwepa mkono wa mamlaka husika.
“Huu ni uhujumu uchumi, iweje majina ya makampuni ya Tanzania yatumike kinyume cha sheria na wafanyabiashara wachache wasio waaminifu?” Alihoji Mtendaji Mkuu wa Masoko wa TPC Ltd, Allen Maro aliwaambia waandishi wa habari.
Waliiomba Serikali kuingilia kati na kudhibiti uingizwaji wa sukari kinyume cha sheria ili kuwawezesha wafanyabiashara halali kufanya kazi na kuhuisha viwanda vya ndani ambavyo wamedai vina sukari nyingi maghalani hivi sasa.