Shirika la viwango Tanzania TBS limeendesha mafunzo maalumu ya ujasiliamali na umuhimu wa ubora wa bidhaa kwa wajasiliamali mkoani Kagera kwa lengo la kuboresha bidhaa zao ili kuendana na ushindani wa soko la dunia.

Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Bukoba hotel ambayo yamewahusisha wajasiliamali Zaidi ya 50 kutoka wilaya za mkoa huo, wajasiliamali hao wameelezwa umuhimu wa kuwa na alama ya ubora(TBS)  kwenye bidhaa zao.

Akifungua mafunzo hayo ya siku moja mkuu wa wilaya Bukoba Deodatus Kinawiro amelishukuru shirika hilo kwa kuamua kuwafikia wajasiliamali kwenye maeneo yao na kuweza kuzijua changamoto zao katika usindikaji wa bidhaa.

Kinawiro amesema kuwa wajasiliamali ni watu muhimu katika ukuaji wa uchumi wa taifa ambao wanatakiwa kusaidiwa kwa kupewa elimu ya ujasiliamali pamoja na namna bora ya utunzaji wa bidhaa tangu zikiwa malighafi hadi kufikia hatua ya kwenda sokoni.

“Wajasiliamali ni watu muhimu kwa taifa letu, TBS mnalo jukumu kubwa sana la kuhakikisha wadau hawa wanapata elimu sahihi na bora yenye lengo la kuwainua katika shughuli zao, tunaona sasa nchi yetu imefikia uchumi wa kati mchango wa watu hawa upo mkubwa.” Ameeleza Kinawiro.

Ameongeza kuwa mkoa wa Kagera unapakana na nchi takribani nne ambazo zinaweza kuwa fursa kwa wajasiliamali wa mkoa huo hivyo wajasiliamali wakikosa alama za ubora kwenye bidhaa zao watakosa masoko kwenye nchi hizo kwakuwa zitakuwa hata hazitambuliki kama ni nzuri.

Aidha Kinawiro amewataka SIDO na TBS kuwasaidia wajasiliamali kupata vifungashio bora ili kuweza kuuza bidhaa zao kwa usafi na ubora na pia waweze kupata faida ambapo amesema kuwa changamoto hiyo imekuwa kero na kuwafanya wajasiliamali kutumia vifungashio visivyobora na kuwapelekea walaji kushindwa kununua bidhaa zao.

Hamisi Sudi ni meneja utafiti na mafunzo kutoka TBS akiongea kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa shirika hilo amesema kuwa wamekuwa wakitoa mafunzo hayo mara kawa mara kwa wajasiliamali nchini lengo ni kuwawwezesha kuzalisha bidhaa zenye ushindani kwenye soko la dunia.

Ameeleza kuwa shirika hilo linaendelea kupambana ili kuhakikisha wajasiliamali wote nchini wanakuwa na alama za ubora (TBS) kwenye bidhaa zao ili kumridhisha mlaji wa mwisho kuiamini bidhaa hiyo kutokana na uwepo wa alama hiyo.

Ameongeza kuwa zipo changamoto kwa wajasiliamali wanaoshindwa kukidhi vigezo vya kuweza kupewa alama na badala yake wanapeleka bidhaa zao sokoni huku wakijua hazina ubora uliothibitiwa na mamlaka husika ambalo suala hilo huwapelekea kukosa masoko ya ndani nan je ya nchi kwa ujumla.

Amewataka wajasiliamali kuwa na tabia ya kuhudhuria mafunzo mbalimbali yanayotolewa na shirika hilo ili kuweza kuwajengea uwezo binafsi wa kuzalisha bidhaa zilizo bora na kuweza kupata masoko makubwa nay a kuaminika.

Wakiongea kwa nyakati tofauti baadhi ya wajasiliamali waliohudhuria mafunzo hayo wamesema kuwa mafunzo waliyoyapata yatawasaidia kuanza kuzalisha bidhaa zenye ubora Zaidi na kuweza kupata masoko makubwa.

Matungwa Daniel ni mkurugenzi wa kiwanda cha Nyaka Food kilichopo Manispaa ya Bukoba ambaye amesema kuwa amekuwa akipata changamoto ya kuuza bidhaa zake nje ya nchi kutokana na bidhaa zake kutokuwa na alama ya ubora (TBS) suala linalompelekea kukosa masoko licha ya kuwa watu kutoka nchi za nje wanazipenda bidhaa zake.

Ameongeza kuwa serikali ikiwasaidia wajasiliamali hao kupata alama ya ubora kwa haraka itawasaidia kupata masoko na kupunguza usumbufu kwao pale wanapokwenda kuuza bidhaa hizo.

Wilaya Bukoba yapungukiwa madarasa 1,297 ya shule za msingi.
Taasisi, mifuko iliyoanzishwa na Mkapa kukabili umasikini