Shirika la viwango Tanzania (TBS), limeendesha mafunzo kwa Wataalamu wa maabara za ubora na uchunguzi kwa lengo la kuwapa ufahamu juu ya vifaa wanavyovitumia katika maeneo yao ya kazi, na kuwataka kuitumia elimu yao kuhakikisha wanafanya upimaji wenye ubora.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila wakati wa ufunguzi wa semina hii leo September 9, 2022 mjini Bukoba, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mosses Machali ameipongeza TBS kwa kuandaa semina hiyo ambayo ina umuhimu kwa wataalamu wa Maabara.
Machali amesema, elimu ya vipimo itaongeza ufanisi katika ufanyaji kazi na kutoa majibu yenye ubora na kuwataka washiriki wa semina hiyo kuzingati mafunzo wanayopewa, kwani yatawasaidia kwenye taasisi zao kufanya upimaji wenye ubora na kuendana na ushindani wa kimataifa.
“Baada ya mafunzo haya tunategemea mkatoe mafunzo kwa vitendo huko kwa wenzenu , niearifiwa kuwa katika semina hii kuna wafanyakazi wa uzalishaji na upimaji katika viwanda, wataalamu wa maabara kutoka hospitali zetu, hivyo hatutegemei mkitoka hapa kuwepo manunguniko kwenye vipimo mnavyokwenda kundelea navyo,” amesema Machali.
Aidha, Machali amewataka washiriki kuzingatia nguzo tano za vipimo sahihi ambapo vipimo na vitenganishi vikifanyiwa uchakachuaji vinaweza kuleta majibu yasiyo sahihi na kusababisha sintofahamu kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa upimaji na huduma za Metrojia shirika la viwango Tanzania, Mhandisi Johanes Maganga amesema semina hiyo itawapa ufahamu zaidi wataalamu kutumia vifaa katika maeneo yao ya kazi na kwamba TBS wanavifanyia vifaa vya upimaji ugezi ili viweze kusoma na kutoa majibu sahihi.
Nao, baadhi ya Washiriki wa semina hiyo, wamelishukuru shirika la TBS kwa mafunzo hayo na kusema yatawasaidia kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao na kuzalisha bidhaa zenye ubora huku wakishauri uwepo wa semina za mara kwa mara zitakazo saidia kujua ubora wa vifaa wananvyotumia na kuvifanyia marekebisho.