Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imepiga marufuku urushwaji angani wa vifaa vya kieletroniki visivyo na rubani (drones) bila kupata kibali maalum.
Kupitia tangazo lake kwa umma, TCAA imesema kuwa kwa taasisi au mtu binafsi kufanya majaribio au kurusha drones, ni lazima apate idhini ya Wizara ya Ulinzi na Usalama pamoja na Mamlaka hiyo.
“Ifahamike kuwa kuanzia sasa, taasisi au mtu binafsi anayetaka kununua, kufanya majaribio au kurusha angani vifaa hivyo visivyotumia rubani anapaswa kupata idhidi ya Wizara ya Ulinzi na Usalama pamoja na kibali kutoka TCAA,” imeeleza taarifa ya Mamlaka hiyo.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari imefafanua kuwa uendeshaji wa shughuli zote za anga nchini uko chini ya Mamlaka hiyo kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.
Tangazo hilo linakuja wakati ambapo kumekuwa na urushwaji wa drones unaofanywa na watayarishaji wa video za muziki kwa lengo la kuchukua picha za juu, pamoja na taasisi mbalimbali zinazochukua matukio husika hasa yanapofanyika katika maeneo ya wazi.
Drones zilitumika zaidi katika uchaguzi wa mwaka 2015 ambapo mikutano ya kampeni za wanasiasa ilikuwa ikipigwa picha za juu kuonesha umati uliohudhuria.