Mamlaka ya Usimamizi wa Anga nchini (TCAA), imesema kuwa sababu iliyopelekea kuzifungia Ndege 3 za Kenya kuja nchini ni kutokana na Kenya kuendelea kuiwekea vikwazo vizito Tanzania na raia wake kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 27, 2020, na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Hamza Johari, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast ya East Africa Radio
“Tumezifungia Ndege za Kenya kwa sababu Tanzania bado inawekewa vikwazo vizito kule kwahiyo na sisi tumerithishwa guilty bila sababu”, amesema Hamza
“Ili kumaliza hili suala ni mazungumzo tu na wao watakapokuwa tayari sisi tutakuwa tayari kwa mazungumzo maana sisi hatuna tatizo la kuzungumza na kuweka mambo sawa lakini lazima wao wawe na utashi wa kufanya hivyo“, ameongeza.
Ndege zilizowekewa zuio ni Air Kenya Express, Fly 540 na Safarilink Aviation ikiwa ni siku chache tu tangu Kenya ilipotoa orodha ya nchi 130 ambazo raia wake wataruhusiwa kuingia nchini humo na hawatokaa karantini huku Tanzania ikiwekwa kando.