Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetaja changamtoto tano za uendeshaji kesi zinazotokana na makosa ya mtandao.
Changamoto hizo zimetajwa kuwa ni uelewa mdogo wa majaji, mahakimu na wanasheria, ushahidi wa kuwasilisha, kufutika kirahisi, uchunguzi, na wapi pa kupeleka malalamiko hayo.
Mwanasheria mwandamizi kutoka TCRA, Dk Philip Philikunjombe amewataka majaji na mahakimu na wanasheria kupata elimu juu ya uendeshaji wa kesi hizo kwani kumekuwa na makosa makubwa yanayotendeka.
Mbali na hiyo amesema bado kuna ugumu wa kujua ni namna gani ushahidi unatakiwa kuwasilishwa mahakamani pindi mtu atakapokwenda kulalamika kuwa katendewa makosa.
”Umetukanwa kwenye simu je upeleke simu ya aliyekuwa kwenye simu, je upeleke simu ya aliyekutukana mahakamani, Tutajuaje kama baada ya kumnyang’anya simu yake hukubadilisha ujumbe. Kama umechapisha katika karatasi, tutajuaje kama hukuongeza maneno au kupunguza? Hivyo, bado ni vigumu kupata ushaidi wa kesi hizi” amesema Philikunjombe.
Lakini pia changamoto nyingine ni ushahidi wa kesi hizo kuharibika kirahisi kwa sababu mtuhumiwa anaweza kufuta ujumbe hivyo haitakuwa rahisi kuthibitisha makosa hata kama ujumbe huo utakuwa nao mlalamikaji.
Kufuatia changamoto hizo wadau mbalimbali wanaotumia mitandao wameshauri wasimamizi wa kesi hizo kupewa elimu ya sheria zinazohusu makosa ya mtandao ili haki iweze kutendeka.