Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imezipiga faini ya Sh38.1 bilioni kampuni sita za simu kwa kutotoa huduma zenye ubora kama ilivyoanishwa kwenye kanuni za ubora wa huduma za mwaka 2018.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Mhandisi James Kilaba wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa imezielekeza kampuni hizo kutozipeleka fedha hizo TCRA badala yake wazitumie katika kuwekeza kuboresha ubora wa huduma ndani ya siku 90.
“TCRA imeazimia kwamba badala ya kulipwa fedha hizo, tuzielekeze kwa watoa huduma. Kila mtoa huduma atumie kiasi chake alichotakiwa kulipa, akiwekeze katika kuboresha huduma.” amesema Mhandisi Kilaba.
“Tunatoa siku tisini na tumekubaliana kwa kusaini hati ya makubaliano maalum, mtoa huduma atakayefanya kinyume TCRA itachukua hatua zaidi za kiudhibiti na kisheria pasipo kutoa taarifa,”
TCRA imetoa adhabu ya faini kwa makampuni ya simu yafuatayo Airtel (Sh11.5 bilioni), Tigo (Sh13 bilioni), Halotel (Sh3.4 bilioni), Vodacom (Sh7.8 bilioni), Zantel (Sh 1 bilioni) na TTCL Sh1.3 bilioni.
Amesema kwa mujibu wa kanuni ya 20 ya kanuni za ubora wa huduma za mawasiliano, mtoa huduma anayeshindwa kufikia vigezo anatakiwa kulipa faini.