Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imekifuta Chuo Kikuu cha Eckernforde kilichopo mkoani Tanga kutokana na kushindwa kukidhi vigezo vya udahili.
Taarifa hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, ambapo amesema licha ya kukifuta chuo hicho, pia vyuo ambavyo havijatimiza vigezo vimepewa miezi sita ya kufanya hivyo ili viweze kufunguliwa.
”Tumekifuta chuo cha Eckernforde, sio tena Chuo Kikuu hapa Tanzania”, amesema Profesa Kihampa.
TCU imekifuta chuo hicho ikiwa ni miezi takribani kumi imepita tangu Septemba 25,2018, ilipotangaza kusitisha utoaji mafunzo na kuamuru wanafunzi waliokuwa wakisoma chuo hicho kuhamishiwa vyuo vingine.
Mbali na kufuta vyuo hivyo vipo vyuo ambavyo vilisitishwa lakini kwa sasa vimerejeshwa mara baada ya kukidhi vigezo na masharti kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Baadhi ya vyuo vilivyofunguliwa ni Chuo kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU), Chuo kikuu kishiriki cha Marian cha Bagamoyo, Chuo kikuu cha kimataifa cha Kampala (KIU) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo (AMUKTA). Huku akiahidi majina ya vyuo vingine vilivyoondolewa kwenye kifungo hicho kutajwa baadaye.
Aidha, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetoa taarifa kwa Umma, Taasisi za Elimu ya Juu na Wadau wote wa Elimu kwamba maombi ya kujiunga na vyuo vikuu hapa nchini kwa Shahada ya Kwanza yameanza rasmi julai 15, 2019 hadi Agosti 10, 2019.
Hivyo imewataka wanafunzi wote wanaotaka kujiunga na elimu ya juu kufanyay udahili na kukidhi masharti yote.